Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, kupitia Kituo cha Umahiri cha Miundombinu ya Maji na Nishati endelevu (WISE-Futures), kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wamefanya ziara katika vyombo vya habari vya radio kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa upimaji wa ubora wa chujio za hewa (airfilter) kwenye magari.   

Ikiwa ni awamu ya pili ya utoaji elimu kwa wananchi ambayo imefanyika katika mikoa ya Lindi na Mtwara kwanzia 11-14 September 2024. Awamu ya kwanza ilifanyika  mikoa ya Dodoma, Mwanza na Mbeya , 13-25 Juni, 2022.

Akizungumza katika ziara hiyo iliyoanza Kiongozi  msaidizi wa Kituo cha WISE-Futures, Prof. Yusufu Chande Jande amesema kuwa, machujio ya magari yasipokuwa na ubora unaotakiwa huathiri magari kwa kuharibu injini ya gari, kutumia mafuta mengi na kuleta athari za kiafya na mazingira.

Kwa upande wake Afisa Viwango wa TBS, Bw. Anorld Mato, alisema kuwa wanashirikiana na NM-AIST kupima ubora huo kutokana na Taasisi hiyo kuwa na maabara ya kisasa ambapo kwa upande wa TBS imeandaa viwango vya ubora wa machujio hayo na kusimamia jukumu la hakikisha ubora wa bidhaa hizo unafatwa.

Alibainisha kuwa, viwango vya upimaji wa machujio hayo ya aina mbili, kiwango cha TZS 3208 cha mwaka 2021 ikiwa ni chujio za kuchuja hewa ya AC, kiwango cha TZS 1959 cha mwaka 2018 ambacho huchuja hewa inayoingia kwenye injini ikiwa ni viwango vya lazima katika bidhaa hizo.

Aidha, Bw. Mato amewataka watengenezaji na waagizaji wa bidhaa hizo kuzingatia viwango vya ubora vilivyowekwa na kufuata sheria zilizopo ili kuepuka adhabu endapo wataenda kinyume na sheria, ikiwepo kurudisha bidhaa kwa nchi iliyotengeneza au kuziharibu bidhaa hizo kwa gharama za muagizaji. 

Naye Mtathimini wa maabara Bw. Hemed Mahim, ametoa wito kwa watumiaji wa bidhaa hizo, kutumia machujio kwa usahihi kwa kuzingatia muda uliowekwa wa matumizi, kuangalia alama ya ubora iliyowekwa kwenye bidhaa ili kulinda afya zao.  

Mnamo Juni 08, 2021, NM-AIST na TBS waliingia makubaliano ya upimaji ubora wa machujio ya magari ili kudhibiti na kusimamia ubora wa chujio za hewa na magari zinazozalishwa ndani na nje ya nchi, ikiwa ni hatua ya kuzingatia afya za watumiaji wa bidhaa hizo hapa nchini.

Kutoka (Kushoto-Kulia) Mr. Arnold Mato kutoka TBS, Mr. Octavian Kanyengele & Prof. Yusufu Chande Jande kutoka WISE-Future na  Bw. Alfred Mlonganile mtangazaji  wa Mashujaa Fm.