Kiongozi wa Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira, kutoka kituo cha umahiri cha miundombinu ya maji, usafi wa mazingira na Nishati endelevu (WISE-Futures) Professa Hans Komakech ametoa wito kwa viongozi wa halmashauri/mji kutumia vizuri taarifa za maji, usafi wa mazingira wanazokusanya ili kuleta manufaa kwa wananchi.

Professa Komakech, ameyasema hayo wakati wa mafunzo ya maji na usafi wa mazingira katika kuwajengea uwezo wataalamu hao kutoka katika Halmashauri za Ludewa, Makete na Mji wa Ifakara  yaliyofanyika kuanzia tarehe 30 Juni,2023 mpaka  08 Julai, 2023.        

Aidha, Professa Komakech anaeleza kuwa WISE-Future imeratibu mafunzo hayo  kupitia ufadhili wa Shirika la Maendeleo  la Kimataifa la Marekani ( USAID) ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa maji na usafi wa Mazingira kwa Mikoa ya Njombe, Morogoro,Iringa na Rukwa.

” lengo la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo wa namna ya kukusanya taarifa, kuzichakata na namna ya  kuzitumia  ili kupanga mpango endelevu wa kuboresha vyoo na upatikanaji wa maji” anasema Professa Komakech

Professa Hans Komakech, akitoa mafunzo kwa washiriki  katika mji wa Ifakara.

                                                               

Vilevile, Professa Komakech amewapongeza Wakurugenzi, Wataalamu mbalimbali kutoka katika Halmashauri, Madiwani na Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji kwa kuweza kuhudhuria kwa wingi na kufanikisha mafunzo hayo.

Naye Mkurugenzi wa Wilaya ya Ludewa Bw. Sunday Deogratius amewashukuru wawezeshaji kutoka WISE-Futures kwa kuratibu mafunzo hayo na kwa Wilaya yake kuwa sehemu ya mradi ambao utasaidia Halmashauri kufanya maamuzi ikiwemo kutambua eneo sahihi la ujenzi wa bwawa la kutibu maji.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ludewa , Bw. Sunday Deogatius akisisitiza umuhimu wa mradi huu kwa washiriki wa mafunzo.

“Naahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wataalamu wote wataopita na kukusanya taarifa hizo ili kusaidia Halmshauri kuwa na matumizi bora ya aridhi,kubaini vyanzo vya maji na kupunguza magonjwa ya mlipuko” alisema Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ifakara Bw. Kassim Nakalapa

Aidha, aliongeza kuwa kupitia Mradi huo utatoa ajira kwa wananchi wa eneo la uchakataji maji na pia kuwa chanzo cha mapato kwa Halmashauri.

Mfunzo hayo yalihusisha ukusanyaji wa taarifa kwa muda wa siku 30 kutoka katika kila Halmashauri/mji na kazi hiyo itafanywa na wataalamu 10 kutoka Ludewa, Makete na Ifakara.

Baadhi ya washiriki wakifanya majaribio ya mahojiano kwa kutumia muongozo uliopo kwenye vishikwambe utakao tumika kukusanya taarifa

Viongozi wa Halmashauri hizo wameombwa kuendelea kutoa ushirikiano zaidi ambapo hatua itakayofuata katika awamu ya pili ya mradi  itahusisha uchukuaji wa sampuli za kinyesi katika vyoo kwa baadhi ya kaya ili kusaidia kuchagua aina ya miundombinu ya kuchakata au kutibu maji itakayofaa katika eneo husika.